Unordered List


Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

Friday, 27 February 2015

Polisi Somalia: Rais hakujeruhiwa katika shambulizi

Polisi Somalia: Rais hakujeruhiwa katika shambulizi
Polisi nchini Somalia imekanusha madai ya kundi la kigaidi la al-Shabab kwamba rais wa nchi hiyo, Hassan Sheikh Mohamud, amejeruhiwa kwenye shambulizi la hapo jana dhidi ya ikulu ya rais mjini Mogadishu.
Kundi la kigaidi la al-Shabab sambamba na kudai kuhusika na shambulizi la hapo jana dhidi ya ikulu ya rais mjini Mogadishu, limesema rais na maafisa wengine wa serikali wamejeruhiwa.  Msemaji wa kundi hilo, Abdiaziz Abu Musab amesema wapiganaji wa kundi lake walivurumisha makombora kadhaa ya mizinga kuelekea ikulu ya rais na baadhi ya makombora yaliingia na kugonga majengo ya ikulu. Polisi ya Somalia imethibitisha kutokea shambulizi hilo lakini ikasema hakuna mtu aliyeuawa au kujeruhiwa. Ali Hussein, afisa mwandamizi katika jeshi la polisi la Somalia amesema uchunguzi unaendelea kubaini wahusika wa hujuma hiyo na sehemu iliyotumika kuvurumisha mizinga hiyo.
Wiki iliyopita kundi hilo la kigaidi lilishambulia hoteli mashuhuri ya Central mjini Mogadishu na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 20 wakiwemo wabunge wawili.

Raia mashariki mwa DRC waanza kurudi makwao


Raia mashariki mwa DRC waanza kurudi makwao
Habari kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinasema kuwa, raia waliokuwa wamekimbia makazi yao kufuatia oparesheni ya jeshi la serikali dhidi ya waasi wa FDLR wameanza kurejea nyumbani baada ya miji kadhaa kukombolewa na jeshi hilo. Habari zinasema wakazi wa mji wa Mulenge ulioko katika mkoa wa Kivu Kusini tangu usiku wa jana wameanza kurejea kwenye nyumba zao baada ya mji huo kukombolewa na jeshi la serikali kutoka mikononi mwa FDLR.
Serikali ya DRC ilianzisha oparesheni kali dhidi ya kundi la FDLR linalowajumuisha waasi wa Kihutu wa kutoka Rwanda wanaopiga kambi mashariki mwa Kongo-Kinshasa. Oparesheni hiyo ilianza siku kadhaa zilizopita baada ya waasi hao kukataa kuweka silaha chini na kujisalimisha kwa hiari. Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa huko DRC MONUSCO ambalo awali lilitarajiwa kusaidiana na wanajeshi wa serikali limekataa kushiriki kwenye oparesheni hiyo

Thursday, 26 February 2015

Bangi ni halali Washington DC

Mji mkuu wa Marekani Washington DC umehalalisha utumizi wa Bangi.
Hatua hii ya Washington inafuatia ile ya jimbo la Colorado, Alaska na Washington state ya kuhalalisha matumizi ya mihadarati kwa starehe.
Mpango huo umekubalika na wananchi wengi katika kura ya maoni iliyopigwa Novemba mwaka jana lakini maafisa nchini
humo wametofautiana na wabunge wa Republican ambao ni wengi bungeni uliosababishwa kusitisha eneo hilo kuidhinisha mbinu za kudhibiti na kutoza kodi mhadarati huo.
Sheria hiyo mpya itaanza kutumika kuanzia saa tano usiku wa Alhamisi na hivyo mtu yeyote atakayekuwa akimiliki bangi kisiri atakuwa huru kuivuta bila hofu ya kukamatwa..
Sheria hiyo mpya hata hivyo imezua tofauti baina ya Meya wa mji huo na bunge la Congress.
Weneyji wa mji huo wenye umri unaozidi miaka 21 watakuwa huru kumiliki gramu 56 ya Bangi.
Meya wa Washington Muriel Bowser
Aidha wanauwezo wa kuipanda majumbani mwao.
Hata hivyo sheria hiyo mpya inaharamisha kuuzwa kwa bangi na ununuzi wake.
Mji mkuu wa Washington DC - ni wilaya maalum lakini haina uhuru na hadhi sawa na majimbo kwa hivyo kuna dhana kuwa ilikiuka kanuni ilipoamua kupiga kura ya maoni.
Katika Barua iliyoandikwa na wajumbe wa bunge hilo la Congress,Meya wa Washington Muriel Bowser ameonywa kuwa sheria za jimbo zinakiukwa iwapo sheria hiyo maarufu itaanza kutekelezwa.
Wajumbe hao wanadai kuwa kulingana na sheria maalum iliyopitishwa na Bajeti ya taifa Kuhalalishwa kwa bangi ni haramu.
Bi Bowser hata hivyo anaendelea kushikilia kukutu kuwa walifwata kanuni zote zilizowekwa.

CHID BENZ ALIPA FAINI 900,000/=, AACHIWA HURU NA MAHAKAMA


 

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imemwachia mwanamuziki Rashid Makwilo 'Chid Benz' baada ya kulipa faini ya sh. 900,000 kufuatia kukamatwa akiwa na madawa ya kulevya.
Chid Benz alikamatwa mwaka jana katika Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam akiwa na madawa ya kulevya, ikiwemo misokoto ya bangi.
Mwanamuziki huyo ambaye alikiri kosa hilo wiki iliyopita, alikamatwa uwanjani hapo akiwa anajitayarisha kupanda ndege kwenda Mbeya kwenye tamasha la muziki.
CHIDI BENZ HURU:Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imemwachia mwanamuziki 'Chid Benz' baada ya kulipa faini ya 900,000/= kwa kukutwa na madawa ya kulevya.

Utumiaji mbaya wa intaneti, changamoto kwa TZ

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa, utovu wa maadili kupitia intaneti katika nchi yake ni changamoto kubwa kwa serikali ya Dar es Salaam. Akizungumza kwenye mahojiano maalum na Idhaa hii, Waziri Mbarawa amesema katika kutatua tatizo hilo, serikali imepitisha sheria ya kukabiliana na uhalifu wa mitandao ikiwa ni pamoja na kuwabana wanaotumia mtandao kueneza mambo yanayokinzana na maadili kama vile kupakuwa na kusambaza picha za uchi na filamu za ngono. Kuhusiana na kutumiwa teknolojia katika kutatua matatizo ya kisiasa nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla, Prof. Makame Mbarawa amesema teknolojia ina nafasi ya aina yake katika kupunguza matatizo yanayojitokeza hususan nyakati za uchaguzi katika nchi za Kiafrika. Amesema maandalizi ya chaguzi mbalimbali barani Afrika kuanzia usajili wa wapigakura, upigaji kura, kuhesabiwa kura na kutangazwa matokeo kunaweza kurahisishwa na kuboreshwa zaidi kupitia teknolojia za kisasa na hivyo kuepusha ghasia na machafuko yanayoshuhudiwa katika nchi za Kiafrika baada ya chaguzi hizo.