Watu wasiopungua 29 wamefariki duniani kufuatia mlipuko wa
maradhi ya kipindupindu huko Sudan Kusini huku mamia ya wengine wakiwa
katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo. Ripoti iliyotolewa na Mfuko wa
Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF imebainisha kwamba, kuna kesi 484 za
ugonjwa huo zimeripotiwa vikiwemo vifo vya watu 29 huku sita kati ya
waliofariki dunia kwa maradhi hayo wakiwa ni watoto wa chini ya umri wa
miaka mitano. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto elfu tano walio chini ya
umri wa miaka mitano, wako hatarini ya kufa kutokana na ugonjwa huo,
ikiwa hatua za dharura hazitachukuliwa. Ugojwa huo ni hatari zaidi hasa
miongoni mwa watoto kwa sababu husababisha mwili kupoteza maji mengi
kutokana na kutapika na kuharisha. Shirika la Afya Duniani (WHO)
linafanya juhudi za kuwahamasisha watu kuhusu jinsi ya kuzuia ugonjwa
huo na pia kutoa chanjo. Mwezi uliopita Wizara ya Afya ya Sudan Kusini
ilitangaza kuwa watu wasiopungua 18 waliaga dunia kwa ugonjwa wa
kipindupindu. Shirika la Afya Duniani(WHO) limetangaza kuwa mwaka jana
mlipuko wa kipindupindu uliiathiri Sudan Kusini ambapo watu zaidi ya
6400 waliambukizwa na 167 miongoni mwao walifariki dunia.
No comments:
Post a Comment