Umoja wa Mataifa umesema kuwa
mshambulizi ya hivi karibuni ya kundi la kigaidi la Boko Haram kaskazini
mwa Nigeria yamesababisha watu zaidi ya elfu 11 kukimbilia Chad katika
siku kadhaa zilizopita. Kundi la Boko Haram tarehe 3 mwezi huu
liliushambulia mji wa Baga unaopatikana katika jimbo la Borno, kaskazini
mashariki mwa Nigeria na kisha kuuteketeza mji huo na vitongoji vyake
visivyopungua 16. Watu wapatao elfu ishirini wanaaminika kuzihama nyumba
zao katika mji wa Baga tangu kundi la Boko Haram liushambulie mji huo
mapema mwezi huu. Ofisi ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa
Mataifa (UNHCR) jana ilitangaza kuwa raia wapatao 11,320 wamewasili
katika nchi jirani ya Chad. William Spindler, msemaji wa UNHCR amesema
kuwa, asilimia 60 ya raia wapya waliowasili nchini Chad walikuwa ni
wanawake na watoto na kwamba watoto 84 wasio na mtu yoyote aliyefuatana
nao pia wamewasili nchini Chad. Ravina Shamdasani msemaji wa ofisi ya
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu (OHCHR) ameeleza kuwa ni wazi kwamba
mauaji ya umati ya raia na kuwalazimisha watu kuhama kwa nguvu vimetokea
katika mji wa Baga nchini Nigeria.
Gazeti
la Charlie Hebdo leo limeanza kusambaza toleo la gazeti lake ambalo
limechapishwa kibonzo cha Mtume Mohammad kwenye ukurasa wake wa mbele.
Nakala Milioni za gazeti hilo zimeanza kusambazwa na nyingine zitafuata iwapo wanunuzi wataongezeka.Picha ya kibonzo hicho iliyopo ukurasa mbele wa gazeti hilo inamwonyesha Mtume Mohammad akilia.
Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa picha hiyo itachochea chuki.
Hata hivyo waandishi wa habari wa gazeti hilo wanasema ukurasa wa mbele unamaanisha Waandishi wa habari wamewasamehe waliotekeleza shambulizi la kigaidi lilolofanyika jumatano wiki iliyopita.
Naibu Mhariri wa Gazeti la Liberalation Alexandra Schwatzbrod anasema ulikuwa uamuzi mwepesi kwa gazeti lake kuchapisha picha ya kibonzo hicho..